BARAZA LA WAFUGAJI NGORONGORO LASHUKIWA KUZIDISHA MUDA MADARAKANI, KIJANA ATAJA ATHARI HIZI
WATETEZI TV
0:00 / 0:00
BARAZA LA WAFUGAJI NGORONGORO LASHUKIWA KUZIDISHA MUDA MADARAKANI, KIJANA ATAJA ATHARI HIZI
2 785 просмотров · 3 недели назад
WATETEZI TV
62,4 тыс. подписчиков
2 785 просмотров · 3 недели назад
Kijana mkazi wa Tarafa ya Ngorongoro Ezekiel Mangi amelilalamikia Baraza la Wafugaji kwa kile alichodai kuwa viongozi wake wameendelea kukaa madarakani baada ya kumalizika kwa muda wa uongozi uliowekwa na Katiba ya Baraza hilo.
Kijana huyo amesema Katiba ya Baraza la Wafugaji inaelekeza kuwa uchaguzi wa viongozi wapya ufanyike kila baada ya miaka mitano, lakini amedai kuwa muda wa viongozi waliopo madarakani umemalizika bila kuitishwa kwa uchaguzi wa nafasi zote za uongozi.
Amesema hali hiyo imeendelea licha ya Baraza la Wafugaji, kupitia Katibu wake James Moringe, kuandika barua Machi 18 mwaka huu kwa kata mbalimbali, ikiagiza kufanyika kwa uchaguzi wa wawakilishi wa vijana, wanawake na viongozi wa mila.
Kwa mujibu wa kijana huyo, uchaguzi wa wawakilishi hao ulifanyika kuanzia Machi mwaka huu, huku wananchi wakitarajia hatua inayofuata kuwa ni uchaguzi wa nafasi nyingine za uongozi, ikiwemo Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina.
Hata hivyo, amesema hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kwa wananchi kuhusu sababu za kutofanyika kwa uchaguzi wa nafasi hizo, hali ambayo amesema imeendelea kuacha uongozi wa zamani ukiwa madarakani wakati tayari kukiwa na wawakilishi wapya waliochaguliwa.
Amesema hali hiyo imeibua mkanganyiko katika utendaji wa shughuli za Baraza la Wafugaji, ikiwemo namna wananchi wanavyopaswa kuwasilisha na kufuatilia masuala yao kupitia viongozi wa baraza hilo.
Ametoa mfano wa wanafunzi wanaohitaji kuomba nafasi mbalimbali kupitia Baraza la Wafugaji, akisema wakati mwingine wanakutana na mkanganyiko kutokana na kuwepo kwa viongozi wa zamani na wapya katika mfumo huo huo wa uwakilishi.
Aidha, amesema wawakilishi wapya wa vijana, wanawake na viongozi wa mila wanashindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa sababu baraza la zamani bado linaendelea kusimamia vikao na maamuzi ya chombo hicho.
Kijana huyo amemtaka Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji, Edward Maura, kutumia busara kwa kuvunja uongozi wa zamani na kuitisha uchaguzi wa nafasi zilizobaki ili kupatikane uongozi mpya unaoendana na matakwa ya Katiba ya Baraza hilo.
Amesema iwapo mwenyekiti huyo hatachukua hatua, wajumbe wapya waliopatikana kupitia uchaguzi wa wawakilishi wa vijana, wanawake na viongozi wa mila wanaweza kutumia nafasi zao kuitisha uchaguzi ili kupatikane uongozi mpya wa Baraza la Wafugaji.
Katika hatua nyingine, amemuelezea James Moringe, ambaye kwa sasa ni Katibu wa Baraza la Wafugaji, akidai kuwa anaendelea kushiriki katika vikao vya maamuzi licha ya kutokuwa diwani, mwenyekiti au mwakilishi wa nafasi nyingine ya uongozi katika eneo hilo.
Amesema hali hiyo inahitaji kuangaliwa kwa kuzingatia Katiba ya Baraza la Wafugaji, akisisitiza kuwa viongozi wanaopaswa kusimamia haki wanapaswa pia kuhakikisha wanaheshimu katiba ya chombo wanachokiongoza.
“Tunataka haki itendeke, Katiba itende haki ya Baraza la Wafugaji. Tunatamani haki ijitokeze kwa watu wenye kudai haki, wajitendee kwanza haki kabla ya kuanza kulalamika kudai haki kwa wengine,” amesema.
Pamoja na malalamiko hayo, kijana huyo ameeleza kuwa hawapingi ushirikiano kati ya serikali na jamii ya wafugaji, akisema wanathamini jitihada za uongozi wa serikali za kukaa pamoja na jamii na kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema baadhi ya changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ni pamoja na upatikanaji wa malisho, maji, barabara na miundombinu mingine.
Pia ametaja hali ya baadhi ya shule katika eneo hilo, akitoa mfano wa Shule ya Msinge ambayo amesema imechakaa na baadhi ya majengo yake kuwa katika hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi.
Ametaka serikali, viongozi wa eneo hilo na uongozi wa shule kushirikiana katika kutafuta suluhu ya changamoto hiyo.
Amesisitiza kuwa wanachotaka si mgongano na serikali, bali mazungumzo yenye tija, ushirikishwaji wa jamii na haki katika uendeshaji wa taasisi zinazowawakilisha wafugaji.
Hata hivyo, amesema hawatakubaliana na kile alichokiita ukiukwaji wa Katiba ya Baraza la Wafugaji, akitaka taratibu zilizowekwa katika Katiba hiyo zifuatwe ili kupatikane Baraza jipya la Wafugaji litakalokuwa na uwezo wa kushughulikia changamoto za jamii na kuziwasilisha kwa mamlaka husika.