WAHUSIKA KWENYE RIWAYA YA NGUU ZA JADI - MTEMI LESULIA
UKETO WA KISWAHILI TV (UWK TV)
0:00 / 0:00
WAHUSIKA KWENYE RIWAYA YA NGUU ZA JADI - MTEMI LESULIA
330 просмотров · 10 мес. назад
UKETO WA KISWAHILI TV (UWK TV)
144 подписчика
330 просмотров · 10 мес. назад
MTEMI LESULIA
Huyu ni kiongozi wa nchi ya Matuo na mumewe Nanzia. Anajitokeza pia kama rafiki shadidi wa Sagilu.
Sifa za Mtemi Lesulia
Mwenye tamaa na ubinafsi
Ni kielelezo cha uongozi mbaya kutokana na jinsi anavyojilimbikizia mali bila kujali raia wake.
Ana tamaa ya kusalia mamlakani; tunamwona anafanya juhudi zote hata kujaribu kuua mpinzani wake ili asalie mamlakani.
Tamaa yake inafanya uchumi wa nchi kuzorota kutokana na sera mbaya za uongozi; akiwa na wenzake, anahujumu pato la nchi kutokana na ubinafsi wake.
Tamaa ya mali inamfanya kujaribu kuwapoka wenyeji wa Matango ardhi yao.
Fisadi
Ufisadi unamfanya Mtemi Lesulia kuajiri watu wasiokuwa na ujuzi au utaalamu katika sekta za umma huku akiacha wale wenye ujuzi (uk. 44).
Serikali yake inaajiri watu kwa kujuana huku ajira zikitolewa kibubusa.
Akishirikiana na wenziwe, anazorotesha uchumi wa nchi kutokana na kutolipa ushuru au kuingiza bidhaa nchini kimagendo.
Ufisadi katika serikali yake unafanya mashirika na taasisi za serikali kumilikiwa na mitandao ya wezi huku akisaidia katika kuipoka nchi hadhi yake.
Katika serikali yake "Ufisadi ulikithiri na maadili yakawapa mkono wa buriani" (uk. 45).
Ufisadi wake pia unajitokeza pale anapowahonga vijana kwenda kumuua Lonare lakini njama hiyo inatibuka.
Anatumia ufisadi kuwahonga watu ili kuwachomea wenyeji wa Matango makao yao kwa lengo la kuwafanya wasimpigie mshindani wake kura wakati wa uchaguzi.
Anatumia njia za kifisadi kuhakikisha kwamba jalada la ardhi ya Matango limefichwa ili kuficha umiliki wa sehemu hiyo.
Pia anawahonga vijana wavuruge amani ili kuharibu kura za mpinzani wa Sagilu wakati wa uchaguzi wa mchujo (uk. 129).
Mdanganyifu
Kupitia kwa uongozi wake, tunaona akidanganya kuwa ardhi ya Matango ingetumiwa kujenga soko ili awafaidi mke wake pamoja na Mbwashu.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu, Lesulia anawadanganya watu waliomtembelea kuwa alikuwa amechoka kuwa mtemi.
Anaposema pia kwamba hakutaka kushinda na kwamba alichoka kuwatumikia anasema uongo (uk. 177).
Katili
Mtemi Lesulia anadhihirisha ukatili pale ambapo anaungana na wengine kumpangia Lonare njama ya kuharibu biashara yake.
Anapompangia njama ya kumuua au hata kufanya atekwe nyara wakati uchaguzi mkuu unapokaribia ni ishara ya ukatili wake.
Hakujali pale watoto na vijana nchini mwake walivyokuwa wakiteseka kutokana na mifumo mibaya ya uongozi wake.
Anahiari wenyeji wa Matango wachomewe nyumba na kuteseka pamoja na jamaa zao ilimradi atimize azma yake ya kunyakua ardhi yao.
Anahiari kujaribu kumfukuza mkewe Nanzia kwa sababu hakuweza kuzaa alipomwoa.
Baada ya kushindwa kesi ya ardhi ya Matango, anamnyang'anya hakimu aliyekata kesi cheti chake cha kazi na kumsimamisha kazi.
Aidha, anamnyang'anya mwanasheria Mafamba cheti cha uanasheria na kumtokomeza kutoka Taria asijulikane aliko.
Anawafukuza marafiki wanaofika nyumbani kwake kumpa pole baada ya kushindwa uchaguzi (uk. 177).
Mnafiki
Kupitia kwa hila zake, anajaribu kuchukua ardhi ya Matango kuwafaidi mkewe Nanzia pamoja na Mbwashu huku akisema serikali ilitaka kujenga soko.
Anajifanya kutojua yaliyomfika Lonare kabla ya uchaguzi mkuu ilhali njama za utekaji nyara wake zilitokana na maelekezo yake.
Mwenye dharau
Anawaita wenyeji wa Matango panya baada ya kuchomewa nyumba zao na kurejea tena katika makao yao (uk.78).
Anaonyesha dharau kwa mwanawe mbele ya rafiki zake anaposema, "Toto hili! Hata sijui lilitoka wapi." (uk.129).
Mwenye ukabila
Utawala wake unatawaliwa na ukabila mwingi. Anawanyanyasa Waketwa na kuwathamini Wakule ambao ni jamii yake. Hili linabainika anapokosa kuwaajiri vijana Waketwa waliohitimu. Hawa wanaajiriwa kufanya kazi za kijungujiko kama vile wafanyakazi katika mashamba ya matajiri.
Anamchukia Lonare kwa sababu huyu alikuwa Mketwa na akafanya kila juhudi ili kumzuia asiweze kuwa mtemi wa Matuo.
Ukabila unamfanya kuhujumu biashara yake hata kumpangia mauti.
Serikali yake inawaajiri watu kulingana na majina yao; aliye na jina la Kiketwa hakuweza kuajiriwa.
Matajiri na wale walio katika ngazi za juu serikalini wanatoka katika jamii ya Wakule pekee na ndio walioweza kuishi katika mtaa wa kifahari kama vile Majuu.
Msaliti
Anaisaliti nchi na watu wake kutokana na uongozi mbaya usiojali maslahi ya wanyonge.
Anaisaliti jamii ya Waketwa kwa kuwatenga katika ajira licha ya kwamba wao pia wanastahili kuwajibikiwa kama Wakule.
Anamsaliti mwanasheria Mafamba aliyefanya kila juhudi za kumfichia maovu ya serikali yake kwa kumnyang'anya cheti cha uanasheria na kumtimua kutoka katika mji wa Taria.
Kitendo cha kumnyang'anya hakimu cheti chake cha uanasheria na kumfuta kazi ni usaliti kwani hakimu alikuwa akitekeleza majukumu ya utetezi wa haki nchini mwake.
Anausaliti uaminifu wa mwanawe Ngoswe kwa kuwataka vijana wenzake kufanya fujo wakati wa uteuzi wa wagombea viti, bila kujali usalama wao.
Anaisaliti imani ya marafiki zake kwa kuwafukuza walipofika kwake kumpa pole baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu.