OTHMAN AWATAKA MADIWANI KUWA MSAADA WA KWANZA KWA WANANCHI
ZANZIBAR YETU
0:00 / 0:00
OTHMAN AWATAKA MADIWANI KUWA MSAADA WA KWANZA KWA WANANCHI
2 961 просмотр · 1 дн. назад
ZANZIBAR YETU
10,9 тыс. подписчиков
2 961 просмотр · 1 дн. назад
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amewataka madiwani kutambua wajibu wao wa msingi katika kuwatumikia wananchi kwa kusikiliza, kufuatilia na kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Othman ameyasema hayo katika Hoteli ya Ocean View, Kilimani, mjini Zanzibar, wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu ya siku tatu kwa madiwani 20 wa chama hicho, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema madiwani wana wajibu wa kufuatilia kwa kina matatizo ya wananchi na kutafuta njia za kuyatatua katika ngazi za serikali za mitaa, akisisitiza kuwa jukumu hilo ni sehemu muhimu ya dhamana waliyopewa na wananchi.
Ameeleza kuwa si jambo linalofaa wananchi kulazimika kupeleka malalamiko yao moja kwa moja kwa viongozi wa juu, wakiwemo mawaziri na Rais, wakati tayari kuna halmashauri na serikali za mitaa zilizoanzishwa kikatiba kwa ajili ya kuwahudumia.
Aidha, amesema madiwani wana nafasi muhimu katika kujenga msingi wa viongozi bora watakaoweza kuhudumu katika ngazi za juu za uongozi wa serikali na kuchangia maendeleo ya taifa.
Amebainisha kuwa mataifa mbalimbali yaliyopiga hatua za maendeleo yamekuwa yakitumia uzoefu na uwezo wa viongozi walioanzia katika ngazi za serikali za mitaa, jambo alilosema linapaswa kuzingatiwa katika kuimarisha maendeleo ya Zanzibar.
Amewataka madiwani hao kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili wananchi na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua ili kutimiza matarajio ya wananchi katika maendeleo ya maeneo yao.
Vilevile, amewashauri kutumia uzoefu wa Zanzibar katika uendeshaji wa serikali za mitaa wa miaka iliyopita kwa kujadili masuala ya uwajibikaji, uadilifu na sababu zinazochangia kupungua kwa ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii.
Amesema ni muhimu kuandaa sera na mikakati sahihi itakayosaidia kuimarisha utendaji wa serikali za mitaa na kuboresha huduma kwa wananchi.
Othman amesisitiza kuwa serikali za mitaa ni sehemu ya mfumo wa kikatiba na si jambo linalotegemea matakwa ya mtu binafsi, akieleza kuwa wananchi wana haki ya kupata huduma kupitia mfumo wa kugawana majukumu kati ya serikali kuu na serikali za mitaa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo upande wa Zanzibar, Omar Ali Shehe, amesema serikali za mitaa kupitia madiwani zina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya wananchi.
Amewataka madiwani hao kutambua pia nafasi yao katika ujenzi wa chama kwa kuzingatia taratibu na kanuni zake pamoja na kushiriki katika juhudi za pamoja za kukiimarisha.
Naye Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Makundi Maalumu, Pavu Abdalla Juma, amesema madiwani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao, zikiwemo migogoro ya ardhi, ubadhirifu na changamoto za kiutendaji.
Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni kutopatiwa nyaraka za vikao kwa wakati na kutoruhusiwa kuondoka nazo baada ya vikao, hali aliyosema inahitaji kuangaliwa ili kuboresha utendaji na uwajibikaji wa madiwani.