Перейти к содержимому

HEKAHEKA ZA MACHINGA, MGAMBO TANDIKA, KWINGINE KUPO HIVI

Mwananchi Digital

0:00 / 0:00

HEKAHEKA ZA MACHINGA, MGAMBO TANDIKA, KWINGINE KUPO HIVI

1 326 просмотров · 23 часа назад
Mwananchi Digital
1,22 млн подписчиков
1 326 просмотров · 23 часа назад
Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz Dar es Salaam. “Hapa msingi mbio” kauli hii imekuwa kama mbiu ya wafanyabiashara ndogondogo wanaokimbizana na mgambo katika maeneo mbalimbali ya Tandika, Dar es Salaam, huku baadhi yao wakisema hawajui kesho watafanyia wapi biashara zao. Katika Mtaa wa Usangi, Leo Septemba 23, 2026 Mwananchi imeshuhudia hekaheka ya machinga wakiuza kwa kuvizia wakati wowote wakitarajia kukutana na virungu vya mgambo kuwatawanya. Hata hivyo Mwananchi imeshuhudia leo wakitawanywa kwa katapira iliyoingia kukwangua barabara hiyo maarufu kwa biashara za wamachinga ambayo imepachikwa jina la m Congo ndogo, ambao ni mtaa maarufu wa Kariakoo. Mwananchi iliyokuwa eneo hilo kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 7 mchana, ilishuhudia meza za wamachinga zikiwa zimebomolewa ikiwa ni mwendelezo wa jiji kuwaondoa katika maeneo hayo na kutaka wahamie maeneo rasmi. Licha ya kubomolewa, waliendelea kuuza mikononi na wengine wakitandika bidhaa zao chini, ilipofika saa 6:30 mchana, Katapira lilipita na kuchimbua barabara hiyo huku likiwatawanya mamia ya machinga na wateja wao ambao baada ya dakika chache katapira hilo kuondoka walirejea tena. Katika eneo hilo ambalo limezungushiwa kamba kuonyesha hairuhusiwi meza au kibanda kuvuka kamba hizo na kuingia eneo la barabara hiyo, ambayo inaelezwa kabla ya oparesheni kuwaondoa wamachinga iliyoanza Jumamosi iliyopita halikupitika kirahisi kutokana na msongamano wa wamachinga na wateja. Baadhi ya wafanyabiashara walieleza hekaheka wanazokumbana nazo dhidi ya mgambo, wakidai si kama hawataki kuondoka eneo hilo, lakini hawana pa kwenda kwani Buza kwa mama Kibonge ambako walitakiwa wahamie hakuna nafasi. "Tuliambiwa twende Buza, lakini kule tulikwama kwa sababu eneo tayari limejaa na tunaambiwa wanaotakiwa kuwa pale ni wale wafanyabiashara waliokuwepo awali ambao ni wazawa na si sisi," amesema Hamis Hamis huku akibubujikwa machozi. Amesema wao si kama wanapenda kukimbizana na mgambo kila siku, lakini hawana pa kwenda, hivyo wanalazimika kurudi eneo hilo na kufanyabiashara kiubishi wakijiandaa kukabiliana na mgambo. Amesema awali waliomba Mtaa wa Usangi utumike kama eneo la biashara kwa kuwa umezungukwa na shughuli nyingine za soko, na wamekuwa hapo kwa miaka mingi kabla ya wiki iliyopita kuvunjwa kwa maeneo yao ya biashara. “Tumepoteza vitu vyetu, tunaishi kwa mateso dhidi ya mgambo, Serikali isingeishia kutuondoa kwa nguvu, itupe na mbadala,” amesema Hamisi. Hata hivyo kwa Tandika changamoto hiyo si mpya, miaka ya 2005 na 2008 waliwahi kukumbana na hali kama hiyo kabla ya kuruhusiwa na kurudi kuendelea na biashara zao. Mfanyabiashara mwingine, Mariam Jumanne amedai wamejikuta katika hali ngumu zaidi kukabiliana na mgambo. “Hatuwezi kuelekea kokote kwa sababu hata huko Buza tulipoambiwa twende tumeenda, tumekuta watu wanapangwa ambao waliokuwepo pale zamani na si sisi,” amesema. Katika eneo hilo, Mwananchi ilishuhudia machinga wakipanga vitu barabarani dakika kadhaa na dakika chache wanaziondoa kupisha oparesheni ya mgambo na kisha kurejea tena, utaratibu ambao wamedai ni wa siku zote tangu bomoabomoa ilipoanza Jumamosi iliyopita. Kiongozi wa wafanyabiashara katika soko hilo aliyekataa kuandikwa gazeti amesema bado wako katika mazungumzo na uongozi ili kuona ni namna gani machinga wa eneo hilo wanasaidiwa. "Watu wameumizwa, hapa hali si hali, ndiyo tupo kwenye mazungumzo na Serikali tuone huli jambo litakwisha vipi, baada ya hapo ndipo nitaweza kuzungumza," amesema kiongozi huyo. Kwingine kupo hivi Wakati wamachinga Tandika wakieleza hayo hali kama hiyo pia imeonekana soko la Mbezi Louis ambako wamachinga wametakiwa kuondoka kwenye maeneo yasiyo rasmi kwa hiari. Mwananchi imeshuhudia katika masoko baadhi ya jiji la Dar es Salaam na baadhi ya Kibaha machinga wakianza kuondoka kwa hiari na wengine kuondolewa kwa nguvu huku wengi wao wakitumia utaratibu wa kuuza mkononi bidhaa zao. Ofisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, Joina Nzala amesema wamekuwa wakitoa elimu ya wamachinga kuhama kwa hiari hadi Septemba 29, 2026, kabla ya kuanza kuwaondoa kwa lazima. Miongoni mwa maeneo hayo ni Simu 2000, Daraja la Kijazi, Kimara Mwisho, Temboni, Stendi ya Kwa Magufuli na Mbezi Mwisho akibainisha maeneo ambayo wafanyabiashara hao hawaruhusiwi kufanya biashara ni pamoja na pembezoni mwa barabara, kwenye mitaro, madarajani na mbele ya maduka ya watu huku wafanyabiashara walio tayari wakitakiwa kutumia masoko rasmi kwa kufuata taratibu. Katika soko la Mbezi Louis, kulikuwa kumejaa meza za wafanyabiashara kiasi kwamba sehemu iliyokuwa ikitumika kama njia haikuwa na nafasi ya kutosha. Mwananchi imeshuhudia meza hizo zikiwa zimeanza kuondolewa na eneo kuwa wazi, licha ya wamachinga kuuza vitu mkononi na wengine kupanga chini hasa nyakati za usiku.