ZANZIBAR YALENGA KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA, SERIKALI YAONGEZA UWEKEZAJI KILIMO
SHUKURU MEDIA
0:00 / 0:00
ZANZIBAR YALENGA KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA, SERIKALI YAONGEZA UWEKEZAJI KILIMO
84 просмотра · 3 недели назад
SHUKURU MEDIA
250 подписчиков
84 просмотра · 3 недели назад
bSerikali ya Zanzibar imesema Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya sekta ya kilimo, huku wakulima na wafugaji wakihimizwa kuachana na kilimo cha kujikimu na kuelekea katika kilimo cha kisasa na cha biashara.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati akifungua Maonesho ya Kumi ya Kilimo ya Nane Nane katika viwanja vya Dole Kizimbani, Wilaya ya Magharibi “A”, Unguja.
Mhe. Hemed amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wakulima na wafugaji kubadilishana uzoefu, kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi.
Amesema ubunifu na elimu zaidi kwa wakulima vinahitajika ili kuongeza uzalishaji, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha usalama wa chakula pamoja na fursa za kuuza bidhaa ndani na nje ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa Mhe. Hemed, Serikali imepiga hatua katika sekta hiyo, ikiwemo kukamilisha mfumo wa Kilimo App, kuongeza usajili wa wakulima, kukamilisha Maabara Mpya ya Utafiti wa Magonjwa ya Mifugo Kizimbani na Kituo cha Masoko ya Mazao ya Nyuki Chamanangwe, Pemba.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, mbegu bora, mifugo, pembejeo, tafiti na matumizi ya teknolojia ili kuongeza uzalishaji na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana na wanawake kwa kuwapatia ujuzi, mitaji, teknolojia na masoko, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ushiriki wao katika sekta ya kilimo na ufugaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Suleiman Massoud Makame, amesema Serikali imeamua kuongeza uwekezaji katika kilimo kwa lengo la kuifanya Zanzibar ijitosheleze kwa chakula na kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje.
Amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau na washirika wa maendeleo imejipanga kuwafikishia wakulima na wafugaji elimu, ujuzi na nyenzo za kisasa ili kuongeza uzalishaji na kupanua shughuli za kilimo na ufugaji.
Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Tanzania, Mhe. Mwasi Damas Kamali, ameipongeza Wizara ya Kilimo Zanzibar kwa kuunganisha sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili katika maonesho hayo, akisema hatua hiyo inawarahisishia wananchi kupata elimu na bidhaa mbalimbali katika eneo moja.
Mhe. Kamali amesema vijana na wanawake wameendelea kuonesha hamasa ya kushiriki katika kilimo na ufugaji, hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele katika mipango ya uwezeshaji.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Saleh Mohd Juma, amesema Serikali imetumia shilingi milioni 750 kuboresha miundombinu na mazingira ya viwanja vya maonesho Dole.
Amesema maonesho hayo yameendelea kukua kwa kuongeza idadi ya washiriki, ambapo mwaka huu jumla ya washiriki 498 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na nje ya Tanzania wanashiriki.
Amewahimiza wananchi kutembelea mabanda ya maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu kilimo na ufugaji wa kisasa, hususan teknolojia zinazoweza kusaidia kupunguza utegemezi wa mvua.
Katika ufunguzi huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pia alitembelea mabanda mbalimbali, akikagua shughuli zinazofanywa na wakulima na wafugaji, pamoja na kupokea maandamano ya magari na vifaa vya kisasa vinavyotumika katika shughuli za kilimo.
Maonesho ya Nane Nane yanaendelea katika viwanja vya Dole Kizimbani, Unguja, yakilenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili, huku wananchi wakipata fursa ya kujifunza teknolojia na mbinu mpya za kuongeza uzalishaji.