Перейти к содержимому

WAZIRI MAZRUI ATANGAZA KITUO CHA KISASA CHA KISUKARI ZANZIBAR!

Tifu Tv

0:00 / 0:00

WAZIRI MAZRUI ATANGAZA KITUO CHA KISASA CHA KISUKARI ZANZIBAR!

895 просмотров · 6 часов назад
Tifu Tv
45,1 тыс. подписчиков
895 просмотров · 6 часов назад
ZANZIBAR WIZARA ya Afya Zanzibar imetiliana saini makubaliano ya ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Matibabu ya Kisukari katika Hospitali ya Mkoa Rufaa Lumumba, kwa lengo la kuimarisha huduma za uchunguzi, matibabu ya kibingwa na udhibiti wa ugonjwa huo nchini. Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland ya nchini Norway kupitia mshirika wa maendeleo Bwana Trond Mohn. Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema kukamilika kwa kituo hicho ni hatua muhimu katika kuboresha huduma kwa wagonjwa wa kisukari na kupunguza madhara yanayotokana na ugonjwa huo. Amesema kituo hicho kitatoa huduma zinazohusiana na matibabu ya kisukari pamoja na elimu kuhusu lishe bora, ili kuwasaidia wananchi kubadili mtindo wa maisha na kuzingatia ulaji unaofaa kwa afya zao. Ameeleza kuwa mabadiliko ya mfumo wa ulaji, ikiwemo kuacha baadhi ya vyakula vya asili na kutumia vyakula visivyofaa kwa afya, ni miongoni mwa mambo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo ya kisukari. Aidha, amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni mwanzo wa hatua muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya kisukari, akiwahimiza wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini ugonjwa huo mapema na kupata matibabu kwa wakati. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, amesema takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha kisukari miongoni mwa wagonjwa waliofanyiwa tathmini hospitalini Zanzibar ni asilimia 16.6, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi na matibabu. Amesema Kliniki ya Kisukari katika Hospitali ya Chumbuni inahudumia wagonjwa 420 wenye kisukari aina ya kwanza na wagonjwa 560 wenye kisukari aina ya pili, huku hospitali nyingine za wilaya zikihudumia wastani wa wagonjwa 250 kila moja. Ameongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2026, Hospitali ya Wilaya ya Chumbuni iliripoti visa 42 vya kisukari wakati wa ujauzito, visa 107 vya vidonda vya miguu, wagonjwa 75 wenye matatizo ya figo na wagonjwa 68 waliopata madhara ya kisukari katika macho. Dkt. Mngereza amesema hali hiyo inahitaji kuimarishwa kwa huduma za ufuatiliaji na udhibiti wa sukari mwilini, akibainisha kuwa ni asilimia 10.9 pekee ya wagonjwa waliogunduliwa kuwa na kisukari wanaofikia malengo ya udhibiti wa kiwango cha sukari mwilini. Hali hiyo huongeza hatari ya kupata madhara makubwa, yakiwemo upofu, magonjwa ya moyo na kushindwa kufanya kazi kwa figo. Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Maradhi ya Kisukari Zanzibar, Omar Abdalla Ali, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa jitihada za kujenga kituo hicho, akieleza kuwa kitasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa wa kisukari. Kituo hicho kinatarajiwa kutoa huduma za uchunguzi wa mapema, matibabu ya kibingwa, mafunzo kwa wataalamu wa afya na tafiti zitakazolenga kuboresha udhibiti wa ugonjwa huo na kupunguza madhara yake. Mradi huo unatekelezwa kupitia ushirikiano wa Wizara ya Afya Zanzibar, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland, Serikali ya Norway na wadau wengine wa maendeleo, huku Kampuni ya RANS Limited ikihusika na ujenzi wa kituo hicho.